Kiungo (michezo)
From Wikipedia, the free encyclopedia
Kiungo (kutoka kitenzi “kuunga”) ni mchezaji ambaye anaunganisha pasi za mipira ya nyuma na eneo la mbele la ushambuliaji ili kufunga goli katika michezo mbalimbali kama vile: mpira wa miguu, ragbi, hoki ya ugani[1].
Viungo kwa jumla hucheza katikati ya mabeki na washambuliaji wa timu yao. Baadhi ya viungo hucheza kwa nidhamu ya ukabaji, kuvunja mashambulizi ya timu pinzani na hujulikana zaidi kama viungo wakabaji. Wengine huwa wanyumbulifu zaidi katika upigaji pasi na hujulikana zaidi kama viungo wachezeshaji au viungo wa juu. Idadi ya viungo katika timu pamoja na majukumu hutegemea zaidi mfumo unaotumika na timu; mjumuisho wa wachezaji hao wakiwa uwanjani hujulikana kwa jina la kati (kwa Kiingereza midfield).[2]
Makocha wengi hupendelea kutumia kiungo mmoja kuvuruga mashambulizi ya timu pinzani, na wengine wakiwa na jukumu la kutengeneza magoli au makujumu sawa ya ukabaji na ushambuliaji. Kwa jumla, viungo ndio wachezaji wanaozunguka sehemu kubwa ya uwanja. Kwa sababu viungo ndio wachezaji wanaomiliki mpira kwa asilimia kubwa wakiwa uwanjani, nafasi hii inahitaji wachezaji walio timamu sana.[3]