Frida Kahlo
From Wikipedia, the free encyclopedia
Magdalena Carmen Frida Kahlo y Calderón (6 Julai 1907 – 13 Julai 1954) alikuwa mchoraji nchini Mexiko. Amejulikana kwa picha zake zinazotumia rangi zenye nguvu na maumbo ya sanaa ya kienyeji ya Mexiko.
Frieda alizaliwa na baba Mjerumani aliyehamia Mexiko na mama mwenye asili ya Kiindio. Alipokuwa na miaka 18 alipatwa na ajali nzito ya basi akaendelea kuishi kwa maumivu kila siku, na hakuweza kuzaa watoto. Aliolewa na mchoraji Diego Rivera, alifanya kazi pamoja naye hata kama huyu hakuwa mwaminifu kwake mara kwa mara.
Picha nyingi zinaonyesha maumivu yake yeye mwenyewe na hali ngumu ya wakina mama. Nyumba alimoishi kati ya miaka 1929-1954 imekuwa makumbusho yake.