Wali
From Wikipedia, the free encyclopedia
Kwa Wali kama cheo tazama "liwali"
Wali ni chakula kitokanacho na nafaka, hasa mbegu ya mpunga inayoitwa mchele, baada ya kazi ya kuikoboa yaani kutoa maganda yake.
Neno "wali" hutumiwa pia kwa nafaka za mtama au ngano zikipikwa, lakini kwa kawaida watu huelewa wali wa mchele.
Wali ni kati ya vyakula muhimu zaidi duniani. Kama chakula cha watu inashindana kidunia na ngano. Hasa watu wa Asia ya Mashariki na Asia ya Kusini hutegemea wali kama chakula cha kila siku.
Katika Afrika wali ni chakula cha pekee kwa watu wengi, isipokuwa pale ambako mpunga unalimwa. Nje ya hapo wali ni chakula cha sikukuu au cha nafasi ya pekee au ya matajiri.
Katika Afrika ya Mashariki chakula kinachopendwa ni kuku kwa wali au samaki kwa wali. Chakula cha pekee kabisa ni pilau ambayo ni wali unaochanganywa na viungo maalumu na nyama.